Ijumaa, 14 Novemba 2014

Athari za sayansi na tekinolojia katika utanzu wa ushairi


Wataalamu mbalimbali wamefasili maana ya fasihi simulizi katika mitazamo tofauti tofauti kama ifuatavyo-;
Balisdya(1983) Fasihi simulizi ni aina ya fasihi ambayo hutumia mdomo katika kuumbwa ,kuwasilishwa na kusambazwa kwa wasikilizaji na watumiaji wake.
Msokile,M(1992). Fasihi simulizi ni kazi ya sanaa inayotumia lugha .Kazi hii huhifadhiwa kwa kichwa na kusambazwa kwa njia ya masimulizi ya mdomo ,hurithishwa kizazi hadi kizazi.
Fasihi simulizi ni sanaa inayotumia lugha ya  mazungumzo ya ana kwa ana ,sauti na vitendo na njia zote za mawasiliano  kufikisha ujumbe kwa jamii.
Massamba(2003)akimunukuu Shaaban Robert anasema ushairi ni sanaa ya vina inayopambanuliwa kama nyimbo,mashairi na tenzi zaidi ya kuwa sanaa ya vina unaufasaha wa maneno machache au muhtasari.
Mnyampara (1970) anasema kuwa ushairi ni msingi wa maneno ya hekima tangu kale ndicho kitu kilicho bora sana ,maongozo ya dunia kwa kutumia maneno ya mkato na lugha nzito yenye kunata iliyopangwa kwa urari wa vina na mizani maalumu.
Ushairi ni kazi ya sanaa yenye kuandikwa au kuimbwa kwa kufuata kanuni za ushairi au kutofuata kanuni za ushairi ikiwa na maana kuwa ushairi waweza kuwa wa kimapokeo au wa kisasa ilimradi ushairi huo uwe unaimbika.
Ushairi kama tanzu mojawapo ya fasihi simulizi haukutoka kwenye ombwe tupu bali una chimbuko  lake ambalo huweza kutueleza jinsi ulivyoanza,kukua na kuenea katika sehemu mbalimbali
Chanzo cha mashairi ni mabadiliko ya kihistoria ya jamii, kisiasa,kiuchumi na kiutamaduni mfano nchini Tanzania matukio kama vile kipindi cha uhuru,azimio la Arusha ,vita vya Kagera ,mfumo wa vyama vingi yamezaa ushairi wa fasihi simulizi ambao unayaelezea matukio hayo kwa undani na athari zake kwa jamii. Migongano ya kitabaka katika jamii nayo ni chanzo mojawapo cha ushairi katika kutatua migogoro hiyo ,watu huzua ushairi unaolingana na hisia zilizo katika mazingira yao. Vilevile shughuri mbalimbali za kijamii kama vile dini ,harusi, sherehe mbalimbali ,misiba zinazua ushairi wake unaolingana na shughuli hizo za kijamii hali ambayo imepelekea kuwa na nyimbo za kanisani ,harusini, jando na unyago na maombolezo.
Sayansi ni mfumo wa kutolea maarifa  katika jamii kupitia kuona na kutenda ilihali teknolojia ni uwasilishwaji wa sayansi hiyo.
Hakuna jambo nzuri lililotokea duniani bila ya kuwa na athari zake .Mafanikio haya ya sayansi na teknolojia mpya yameleta athari kubwa sana katika fasihi simulizi na tanzu zake zote hususani utanzu wa ushairi na vipera vyake kama ifuatavyo;-
Nyimbo ni sanaa yenye dhima kubwa katika jamii ,hutumika kuburudisha watukwenye sherehe au wakati wa mapumziko ,kuonya ,kufunza, kuarifu kunogesha hadithi,kuomboleza ,kubembeleza mtoto ili alale,kuchapua kazi na kutia hamasa vitani .Nyimbo hizi zilianza kutumika toka binadamu alipoanza kupambana na mazingira  yake. Shughuli  mbalimbali za uzalishaji mali pamoja na shughuli za kijamii ziliwafanya watu waibue nyimbo mbalimbali kutokana na hisia za kibinadamu katika kutaka kutawala jamii yake na shughuli zake za kila siku.Kabla ya kuja kwa wakoloni na maendeleo ya sayansi na teknolojia tulikuwa na nyimbo zetu za asili ambazo ziliimbwa kufuatana na kazi waitendayo kwa lengo la kuchapuza kazi hiyo .Kila kazi katika enzi za mababu zetu ilikuwa na nyimbo zake , mfano kilimo(wawe),kutwanga,kupepeta,kusuka,kuchuuza,useremala,uvuvi,ubaharia(kimai),uashi,ufugaji,ufuaji chuma na uhunzi.Pia kulikuwa  na nyimbo za watoto kwa lengo la kubembeleza watoto wakati mama afanyapo kazi ambapo  nyimbo hizo zilikuwa na uwili ambapo maudhui yalikua ya kiutu uzima na fani ilikuwa ya kitoto.Kila kabila ilikuwa na aina yao ya kubembeleza watoto vile vile  kulikuwa na nyimbo ambazo ziliimbwa wakati wa kupeleka vijana jandoni na unyagoni.Lengo la nyimbo hizi ni kuwatia moyo na kuwapa ushupavu na ujasiri.Pia kusisitiza dhima mpya ya kiutu uzima na kuuaga utoto,mfano wa wimbo  wa jando uliokuwa ukiimbwa zamani
                               ‘’Netumwa kiazi tungu
                                 Nachimba cha mnyelele
                                  Kizongozongo mabuyu
                                  Ndani kinauchelele
                                  Ukikichocha hakigwi
                                 Kitunga mambelembele
                                 Kitamu sili na ndugu
                                 Jirani simtoche(le)
                                Kitiwacho sitarani
                                Funga na lengo komele……’’
Kutokana na kuibuka kwa sayansi na teknolojia  nyimbo zimepoteza uasiliawake kutokana na kuwepo kwa vifaa vya kisasa.Nyimbo zimeathiriwa na sayansi na teknolojia mfano  badala ya mama kumbeba mtoto mgongoni na kumbembeleza ili alale, kumeibuka  vifaa  mbalimbali  vya  kubembeleza watoto. Vifaa hivi vinafanya kazi aliokua akiifanya mama kwa mtoto, mfano wa vifaa hivyo ni baisikeli ,simu,  filimbi ,vinanda, bembea na mwanasesele. Vifaa hivi  vimeathiri na kupoteza uasili wa nyimbo zetu ambazo zilikuwa zikitumiwa na mama zetu katika kubembeleza watoto.Pia uwepo wa sayansi na teknolojia umesababisha kuongezeka kwa maradhi   ambayo  yamepelekea shughuri za jando na unyago kufanyikia Hospitalini na kupelekea kutoweka kwa  nyimbo ambazo zilikuwa zikiimbwa katika  shughuli hizo za jando na unyago. Uwepo wa sayansi na teknolojia umeleta athari pia katika nyimbo za maombolezo ambapo badala ya watu kukaa na kumfariji mfiwa kwa kutumia nyimbo za asili sasa watu hutumia luninga ,nyimbo za dini  mbalimbali au hata nyimbo za bongo fleva.
Ushairi ni utanzu wa fasihi simulizi unaowasilishwa kwa hadhira kwa njia ya uimbaji au ughani badala ya usemaji wa kawaida. Vigezo vilivyotumika katika kugawa utanzu huu ni kigezo cha lugha ambacho ni lugha ya kishairi.  Kigezo cha pili ni fani ambayo fani iliyotumika ni wizani,lugha ya mkato, lugha ya mafumbo na uimbaji au ughani .Katika utanzu huu kuna vipera viwili ambavyo ni nyimbo na maghani .Kabla ya ukuaji wa sayansi na teknolojia mashairi yalitambulika kupitia sifa zake bainifu ambazo ni urari wa vina na mizani na urari wa mapigo, hivyo ilimlazimu mtunzi wa mashairi kutumia sifa hizo katika kutengeneza kazi yake ya fasihi na mashairi yaliyokuwa yakitungwa yalikuwa yakisifia utawala, mambo ya kishujaa yaliyofanyika katika jamii, kutoa wosia kwa vijana ,kuhamasisha jamii na mshairi alisifika kutokana na ufundi wake wa kutunga na kughani mashairi. Mfano


Lakini kwa sasa kutokana na ukuaji wa sayansi na teknolojia, sifa za urari  wa vina na mizani si muhimu kilicho muhimu ni maudhui yanayozungumuziwa ndani ya ushairi au maghani .Hii ni kutokana na kuongezeka kwa washairi ambao wamekuja na mfumo mpya wa utungaji wa mashairi bila kuzingatia urari wa vina na mizani .Mfano waimbaji wa muziki  wa kizazi kipya ambao hutunga mashairi mengi yanayojali maudhui  bila kuzingatia urari wa vina na mizani .Ukweli huu unadhibitika katika shairi la ‘’Ndiyo  mzee’’ liliyoandikwa na Professor Jay
‘’OK, OK naitwa Joseph Haule mwana Msolopaganzi
Nadhani nimeletwa kuokoa hiki kizazi
Mimi ni mwanasiasa aliyebarikiwa na Mungu
Nimeletwa kwenu waungwana niwapunguzie machungu
Mimi ni mteulekusini mwa jangwa la sahara
Ndio maana nimetunukiwa  cheti cha juu cha utawala
Nina hekima kuliko mfalme suleimani msiwe na wasi
Na hii nitadhihirisha pindi mtakapo nipa nafasi
Actually nimedhamiria kuwasaidia
Taifa lenye  nguvu  duniani liwe ni Tanzania.’’
Katika  kipindi cha awali uhifadhi wa mashairi kama kazi ya sanaa ulikuwa katika ubongo wa fanani ,ambapo fanani katika utendaji wa kazi yake  alionana ana kwa ana na hadhira na uwepo wa hadhira ulipelekea utendaji wa kipera hiki kuwa hai. Lakini  katika kipindi hiki  cha maendeleo ya sayansi na teknolojia kazi hii ya kisanaa haihifadhiwi katika kichwa cha fanani bali huhifadhiwa katika vyombo vya kisasa kama vile vinasa sauti,tanakilishi ,CD za picha na maandishi hivyo si lazima fanani kuonana na hadhira.
Maghani ni ushairi unaoganwa au kuimbwa hadharani. Mara nyingine sauti ya maghani huwa ni kati ya uzungumzaji na uimbaji .Katika enzi za mababu zetu maghani zilikuwa za masimulizi na zilitambwa hadharani pamoja na ala ya muziki kama, vile ngoma na marimba na zilitambwa bila ala ya muziki. Maghani hizi zilizungumzia masuala mazito ya kijamii au ya kibinafsi na zilikuwa ndefu sana zenye kusimulia hadithi au historia, zilikuwa zimegawanyika katika ghani za nafsi ,ghani tumbuizo ,sifo na ghani masimulizi. Maghani  Hizi zote zilikuwa zikielezea masuala mbalimbali yaliyokuwa yakitokea katika jamii .Mfano wa maghani sifo walizokuwa wakitumia mababu zetu ni zile za Fumo lyongo na Mwanakupona. Mfano  wa maghani ya Fumo lyongo ni kama vile;-
‘’Lyongo kitaka mali
Akababalighi rijali
Akawa mtu wa kweli
Na haiba kuongeya
Wagala wakabaini
Kumwambia sulutwani
Twamtaka kwa thamani
Kijana kutuweleya
Twaitaka mbeu yake
Nasi kwetu tuipeke
Kwa furaha tumuweke
Apate kutuzaliya’’
Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia mfumo wa utambaji wa maghani wa zamani umepoteza uhalisia wake, kwa sasa mghani hurekodi mapigo mbalimbali yanayoendana na kazi yake. wakati wa kughani mghani huhitaji  mapigo au ala yaliyorekodiwa na kuhifadhiwa kwenye vyombo vya kisasa kama vile santuri na kanda za kunasia sauti ambazo humurahisishia mghanaji (mghani) kufanya kazi yake vizuri. Mfano wimbo wa ‘’Nikipata nauli’’ uliotungwa na Mrisho Mpoto.
Pole sana mjomba
Kwa kibarua kizito  
’cha kutaka kubadili
Dunia kuwa kijiji
Hongera
Kile kiitikio cha
Globalization kimeimbwa  
Vizuri sana,japo
Hakijakaririwa
Na sikia wageni wamefurahi
Sana na ule ubeti wa mwisho
Uliouongeza wa mbio zetu
Toka uhuru mpaka hapa tulipo’’
Ngonjera ni tungo za kishairi ambazo huwa na muundo wa majibizano. Utungo huwa ni wakimazungumzo unaoweza kuhusisha malumbano au kujibizana kwa nia ya kutoa ujumbe Fulani. Mhusika mmoja anaweza kusana jambo moja katika ubeti mmoja na mwingine kujibu. katika jamii za kiafrika kuna aina ya ushairi wa fasihi simulizi unaoweza kuhusihwa na ngonjera  ambapo mtunzi mmoja husema jambo ambalo wenzake wanaliendeleza. Kwa njia hii kunakuwa na aina ya majibizano kati ya wahusika, mfano ngonjera zilikuwa zikiimbwa  katika sehemu za pwani hasa Lamu na Zanzibar pia jamii nyingine ziliimba ngonjera sehemu mbalimbali kama vile harusini, katika sherehe za kiutamaduni na ngonjera hizo ziliwasilishwa kwa njia ya mdomo. Katika kipindi cha mababu zetu ngonjera hizi ziliimbwa katika mazingira halisi yaliyohusisha fanani na hadhira walikuwa wakionana ana kwa ana wakati wa uimbaji wa ngonjera. Kutokana na uwepo wa sayansi na teknolojia ngonjera hizi  za zamani zimepoteza hadhi yake na kupoteza uhalisia wa kiafrika hali ambayo zimebadilika na kuchukua  uhalisia wa kizungu. Pia ngonjera za siku hizi zinaimbwa kwa ajili ya kuendeleza siasa na mapenzi.


Kwa ujumla ushairi huweza kufa kutokana na mabadiliko ya kijamii, kisiasa kiuchumi na kiutamaduni. Mabadiliko hayo husababisha kitu cha zamani kife au kitu kipya kiibuke kutokana na hali hii sayansi na teknolojia imesababisha nyimbo za zamani kufa kutokana na muda wake kupita au kuisha na badala yake zimeibuka nyimbo mpya katika tasinia ya leo. 
















Alhamisi, 13 Novemba 2014

michakato ya kimofolojia inavyotumika kuunda maneno katika lugha ya kiswahili.



Mofolojia ni taaluma inayoshughulikia vipashio vya lugha na mpangilio wake katika uundaji wa maneno. Vipashio hivyo vya lugha huitwa mofimu (Rubanza, 1996).
Mofolojia ni tawi la taaluma ya isimu ambalo huchunguza maumbo ya maneno na hususani: maumbo ya mofimu. (Mathews, 1974)
Hartman (1972) anasema kuwa mofolojia ni tawi la sarufi ambalo hushughuliia na uchunguzi na uchambuzi wa maumbo, fani na aina zao maneno yalivyo sasa pamoja na histori zao.
Mofolojia huchunguza mofimu na alomofu zake fulani na jinsi ambavyo hukaa pamoja kuunda maneno mbalimbali katika lugha zinamotumika (Richard na wenzake 1985).
Kwa ujumla, mofolojia ni tawi la isimu ambalo huchunguza maneno ya lugha fulani na aina zake za maneno hasa upande wa upangaji wa mofimu mbalimbali zitumikazo kwa ajili ya kuunda maneno. Pia wana taalamu mbalimbali wamefasili maana ya maneno kwa mitazamo mabalimbali kama ifuatavyo.
Tuki, (1970) Neno ni mkusanyiko wa sauti ambazo huweza kutamukika na kuandikwa kwa pamoja na kuleta maana.
Massamba na wenzake (2003) wanafasi neno kwa kutafasili maelezo ya Lynos (1968:194- 208) kuwa neno linawez kufafanuliwa katika misingi ya kiumbo sauti yaani kwa kuchunguza sauti zinazounda umbo zima, kiontografia kwa kuchunguza herufi zinazotumika katika kuliandaka umbo lake, kisarufi kwa kuchunguza kile kinachowakilishwa na umbo husika katika lugha.
Katika lugha ya Kiswahili, maumbo ya kimatamshi na ya kimaandishi huweza kuwakilisha umbo moja au maumbo kadhaa ya kisarufi. Mfano,  katika lugha ya Kiswahili kuna umbo la Kimaandishi kaa. Kisarufi umbo hili linawakilisha maumbo matatu yenye maana tofauti kama ifuatavyo.
Kaa- tendo la kuketi kitako
Kaa- aina ya samaki
Kaa- kipande cha ukuni chenye moto au kilichochomwa.
Kwa ujumla, neno ni sehemu ya lugha yenye kituo kidogo mbele na nyuma yake, au kwa maandishi ni jumla ya herufi zenye maana zilizotengwa kwa nafsi nyuma na mbele.
Maneno katika lugha ya Kiswahili huweza kuundwa kupitia michakato mbalimbali kama vile kimofolojia, na kifonolojia, kwa kutumia mchakato wa kimofolojia, neno huweza kuundwa kupita kanuni mbalimbali kama vile, udondoshaji, uyeyushaji, Muungano wa sauti, nazali kuathiri konsonanti, konsonanti kuathiri nazali, Ukaakaishaji, usilimishaji au usilimisho na mchato wa msinyao.
Katika mchakato wa udondoshaji, kiambishi awali m- ambacho huonekana katika umbo la nje la maneno kama mu- tu, mu- gonjwa, mu – kanda. Katika kanuni au mchakato huu wa undoshaji. Irabu “u” hudondoshwa pale inapofuatiwa na konsonanti halisi katika mpaka wa mofimu. Mfano.
Mu+ tu= mtu
Mu+ gonjwa= mgonjwa
Mu+ kanda= mkanda
Mu + guu = mguu
Mu + china= mchina
Mu+ kulima = mkulima.
Pia irabu ‘u’ inapokalibiana na irabu inayofanana nayo hubaki kama ilivyo.Mfano
Muumba-  muumba
Muumini- muumuni
Muuguzi- muuguzi
Mungwana- muungwana
Muunguja- muunguja.
Mchakato wa uyeyushaji, kanuni hii hutokea pale irabu inapoandamana na nazali “m” na pale inapokuwa yenyewe. Irabu ‘u’ inapofuatiwa na mofimu inayoanza na irabu inayofanana nayo hubakia jinsi ilivyo lakini inapofuatiwa na irabu isiyofanana nayo wakati mwingine huweza kubakia kama ilivyo au huweza kugeuka na kuwa ‘w’ pia irabu ‘I’ huathiriwa na kanuni hii mfano
Mi+ ake- myaka
Vi+ ake- vyake
Vi+ ao- vyao
Vi+ akula          vyakula
Pia katika kanuni hii neon likitamkwa kwa haraka uyeyushaji huweza kutokea. Mfano;
Mu+e+nde+shaji          mwendeshaji
Mu+i+mba+ji              mwimbaji
Mu+ema                      mwema
Mu+eupe                     mweupe
Katika kanuni hii iwapo kuna namna mbili za utamkaji inaashiria kuwa katika mazingira hayo kanuni ya uyeyushaji ni ya hiyari.
Machakato wa muungano wa sauti, kanuni hii hutokea pale ambapo irabu ya mofimu moja inapokabiliana na irabu ya mofimu nyingine irabu hizo mbili huungana na kuzoa irabuy moja tu mfano
Wa+ ingi- wengi
Me +ingi- mengi
Hapa ina maana kuwa irabu ‘a’ na irabu za mbele yaani ‘i’ na ‘e’ zinapokutana katika mpaka wa mofimu huungana na kuzaa irabu moja tu ‘e; lakini kuna vigaili amabapo hutokea inapokuwa mofimu inayoiandama ina minyambuliko. mfano
Wa+ igi+za+ ji - waigizaji
Wa+ oko+ a+ ji-  waokoaji
Mchakato wa nazali kuathiri konsonanti andamizi, katika kanuni hii baadhi ya sauti ambazo huathiriwa na nazari inapokuwa sauti hizo zinazoindamia nazari hizo. mfano.
                        n+ limi- {ndimi}
n+ refu- {ndefu}
Katika mifano hii inaonekana kwamba sauti/ l/na/r/ zinapotanguliwa na nazari “n” hugeuka na kuwa sauti/d/
Mchakato wa konsonanti kuathiri nazali,katika lugha za kibantu umbo la nazali huathiriwa na konsonanti inayoind amia. kwa mfano
Nguzo- [inguzo]
Ngao-[ ingao ]
Katika mifano hii konsonanti inayofuatia nazali ni “g”. konsonsanti hii hutamkiwa nyuma  kwenye kaakaa laini, kwa maelezo haya….. haitokei hivihivi bali ni kutokana na kanuni hii maalumu ya lugha nyingi za kibantu ambazo ni kanuni ya konsonanti kuathiri nazali. 
Mchakato wa ukaakaishaji  wa fonimu,  hutopkea wakati ambapo fonimu zisizo za kaakaa gumu zionapobadilika na kuwa fonimu za kaakaa gumu. Katika lugha ya kiswahili fonimu za kaakaa gumu ni mbili yaani vizuiwa kwamizwa ambavyo ni ?t? na ?ts? kwa hiyo katika lugha ya kiswahili ukaaishaji wa fonimu hutokea wakati ambapo fonimu zisizo vizuiwa kwamizwa hubadilika na kuwa vizuiwa kwamizwa. Ukaakaishaji katika lugha ya Kiswahili hutokea zaidi katika vivumishi, nomino na vitenzi .
ukaakaishaji katika  vivumishi hutokea  katika mipaka ya mofu  za vivumishi, vivumishi vinavyohusika ni vile ambavyo mizizi huanzia na irabu. Kiambishi awali pekee ambacho husababisha ukaaishaji katika lugha ya kiswahili ni kiambishi/ ki/. Kiambishi / ki/ kinapowekwa pamoja na vivumishi ambavyo mizizi yao inaanzia na irabu ‘u’ ukaakaishaji hutokea
mfano
vivumishi vimilikishi
-angu- ki+angu- kyangu- chyangu- changu
-etu- ki+etu- kyetu- chyetu- chetu
Katika kanuni hii kizuiwa hafifu/k/ ambacho hutamkiwa kwenye kaakaa laini hubadilika kuwa kuzuiwa kwamizwa / ts/ ambacho hutamkwa kwenye kaakaa gumu.
Ukaakaishaji katika nomino, hutokea katika nomino chache za Kiswahili
Mfano
-ki+akula- kyakula- chyakula- chakula
-ki+ombi- kyombo- chyombo- chombo
Ukakaishaji katika vitenzi, hutokea pale ambapo mofu {ki} inapowekwa pamoja na mofu {o} ya urejeshi.
Mfano
{A} + {li} + {ki} + {o} + {ki} +{let} +{a}
1                  2         3       4         5         6           7
{A}+{li} + {cho}_ {ki}+ {let} + {a}   ambapo {ki} + o  cha
1       2                   3      4        5      6
Mofu ya tatu {ki} na ya nne {o} zinaungana na wakati  huohuo panatokea ukaakaishaji ambapo /k/ ina kaakaishwa na kuwa /ts/
Usilimisho pamwe wa nazali kanuni hii inahusu maathiriano ya mofimu zinazofuatana. Maathiriano haya huzifanya mofimu zifanane zaidi kuliko zikiwapelekee katika lugha ya Kiswahili ngeli ya 9, 10 na 11. Ngeli ya 9 umoja naya 10 uwingi  hujulikana kama ngeli ya nazali au kingo’n go. Ngeli ya 11 umoja uwingi wake ni ngeli ya 10

Mfano, N+ goma- {ngoma}
             N+ dizi- {ndizi}
             N+ buzi – {mbuzi}
           N+ geli- {ngeli}
           N + bingu – {mbingu}
Mifano hii inaonesha kuwa mofimu ng’ongo ambayo ni /n/ na /m/ hutokea kutegemea na sauti inayoanza katika mzizi Rubanza (1999) .
Vilevile Mgullu(1999) anajadili usilimisho pamwe wa nazali kutegemea usilimisho ambao fonimu jumuishi huupata. Usilimisho huu, hueleza kuwa hutegemea mahali ambapo konsanti inayofuata fonimu jumuishi hutamkiwa. mfano hutokea kama /n/ - /d/ katika maneno, ndizi, ndama, yaani fonimu jumuishi /n/ hutokea kama  /n/ katika maziongira kabla ya /d/
Pia hutokea kama /m/ - /b/ katika maneno mbuzi mbali yaani fonimu jumuishi /n/ hutokea kama /m/ katika mazingira kabla ya /b/. Lakini mtazamo huu una utata haungwi mkono moja kwa moja kuwa /n/, /m/ ni sauti tofauti za mofimu jumuishi moja.  Huenda ikaja kutokea, baada ya uchunguzi, kuwa labda hizi ni fonimu tofauti ambazo labda zina fanana kidogo kwa sababu zote zina unazali.
 Kwa ujumla, michakato inayotumika katika lugha ya kiswahili imesaidia sana katika uundaji wa maneno ili kufanikisha baadhi ya maneno kutamkwa baada ya kutoka umbo la ndani na kwenda umbo la nje ambalo hutokana na lugha mbalimbali za kibantu kutopkana na athari zitokanazo na utamkaji ndizo zimesababisha kutokea kwa kanuni mbalimbali ili kuweza kusababisha matashi na maumbo ya herufi mbalimbali hutamkiwa sehemu yake inayohusika.

 MAREJEO
 Tuki, (2004), kamusi ya Kiswahili sanifu. Oxford University press: Nairobi.
Mgulu, R..S (1999), Mtaala wa Isimu: Fonetiki, Fonolojia na Mofolojia ya Kiswahili. Longhorn Publishers Ltd: Nairobi.
Massamba, D.P.B (2001), Maendeleo Katika Nadharia ya Fonolojia. Taasi ya taaluma za Kiswahili (Tuki): Dar es salaam.
Habwe, J na peter, K (2004), Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Phoenix Publishers: Nairobi.
Massamba na wenzake, (2003), Sarufi Mauumbo ya Kiswahili Sanifu (SAMAKISA) Sekondari na vyuo. Taasisi ya uchungazi wa Kiswahili: chuo kikuu cha Dar- es – salaam.
Rubanza. Y. I (1999), Mofolojia ya Kiswahili, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania: Dar es Salaam.